
WABUNGE wa Bunge Maalumu la Katiba wametakiwa kuona wana deni kwa Watanzania la kuwapatia katiba nzuri ambayo italeta ustawi kwa miaka mingi ijayo. Hayo yalisemwa jana na Dora Mpilimbi ambaye ni balozi kiongozi katika kitongoji cha Chinangali mtaa wa Nala kata ya Nala wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi.
Alisema ni muhimu kwa wajumbe wa Bunge hilo kuona wana deni kwa Watanzania la kuwapatia katiba iliyo nzuri kwa maslahi ya nchi kwa miaka mingi ijayo.
“Waweka mbele maslahi ya Taifa kwani sasa macho na masikio ya Watanzania yako kwao tunatarajia kuona inapatikana katiba nzuri ambayo itakuwa na misingi mizuri,” alisema.
Pia alisema ni muhimu katiba hiyo ikaimarisha muungano wa serikali mbili badala ya kufikiria kuwa na serikali tatu.
“Kuongeza Serikali ya tatu sioni faida yake kutakuwa na maamuzi yatakayofanya kushindwe kuamua baadhi ya mambo, bora serikali mbili ambazo tumekuwa nazo siku nyingi,” alisema.
Akizungumzia suala la posho za wajumbe hao wa bunge maalumu la katiba, alisema fedha wanayolipwa ni nyingi sana.
“Fedha wanazolipwa kwa siku ni nyingi sana sisi maskini wala hatuelewi, mbona hela zote wanachukua wao, tutaondoshaje umaskini kwa hali hii wakati kuna baadhi ya watu wanajali zaidi maslahi yao,” alisema.
Alisema ni vyema kwa wajumbe hao kuweka mbele utaifa na maslahi ya chama baadaye ili kuwezesha kupatikana kwa katiba nzuri ambayo itawakomboa Watanzana katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Iyumbu Dodoma mjini, Yona Ngobito amewataka wajumbe wa Bunge maalumu la katiba ambao wameteuliwa na Rais kujiepusha na tabia ya kufanya fujo kwa kuwa wakifanya hivyo wanaudhalilisha uteuzi wao na kutoheshimu uteuzi wa Rais.
Alisema hayo wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi na kutaka Wajumbe wote kuheshimu sheria na taratibu zilizopo wanapokuwa ndani ya Bunge hilo, ili waweze kuleta matumaini ya Watanzania ambao hivi sasa wamechoshwa na tabia za ukosefu wa nidhamu unaofanywa miongoni mwao.
Alisema hata kama kanuni na sheria hazijapatikana bado wajumbe hao wanatakiwa kufahamu kuwa nidhamu ni jambo la kuzingatia na watambue serikali imetumia gharama nyingi za mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutatua baadhi ya kero za wananchi.
CHANZA:HABARILEO
No comments:
Post a Comment