Na Mbega Mnyama
Hapo kale, katika kijiji cha Iyamba, palizaliwa watoto wawili mapacha. Wazazi wao ambao walikuwa wakulima stadi, walijawa na furaha zisizo kifani. Wakaamua kuwaita watoto wao Sima na Shubila. Wakati wa utoto Sima na Shubila walipenda kufuatana na wazazi wao shambani. Walifurahia kazi za kilimo. Jinsi walivyozidi kukua ndivyo tamaa yao ya kupenda kilimo ilivyoongezeka.
Nyuma ya nyumba yao walianzisha bustani ndogo ndogo za mboga kama vile mchicha, biringani, nyanya na vitunguu. Wazazi wao walifurahia sana vitendo vya watoto wao, hivyo walikuwa tayari kuwapa msaada wowote waliohitaji katika kazi zao za bustani. Siku moja Bwana Mganga wa Kituo cha Afya aliwasili kijijini kununua mboga za wagonjwa. Pale kijijini hakuwapo mtu yeyote aliyekuwa na mboga isipokuwa wale watoto wawili.
Wakati huo Sima na Shubila walikuwa shuleni, hivyo wazazi wao wakaziuza zile mboga kwa niaba ya watoto wao. Wakapata shilingi thelathini. Sima na Shubila waliporudi nyumbani, walionyeshwa zile fedha zilizopatikana, wakafurahi. Habari hizi zilipoenea katika kijiji watu hawakuamini. Baada ya kupata fedha hizo, wazazi wao wakawanunulia uma ya kulimia na bomba la kumwagilia maji. Fedha zilizobaki wakawawekea akiba katika benki ya posta. Watoto wakaendelea kufurahia mazao ya kazi yao.
Wakatambua ubora wa kazi za kilimo. Tabia yao shuleni ilikuwa mfano bora kwa wanafunzi wenzao kwani walipenda sana kazi za kilimo. Kila mara mwalimu alipotoa kazi za shamba, wao walikuwa wa kwanza kabisa kushika majembe na kuzifanya kazi hizo kwa furaha. Juhudi zao katika kilimo ziliwafanya watoto wengine wafuate mfano wao. Hawakuonyesha bidii katika kilimo tu, bali hata katika kazi za darasani na michezo mbalimbali. Kwa ajili hiyo walipendwa sana na walimu na wanafunzi wenzao.
Wakati Azimio la Arusha lilipotangazwa, Sima na Shubila walikuwa wamekwisha anza kujitegemea. Siku moja mwalimu mkuu wa shule alimwalika Bwana Shamba shuleni kuja kuwaeleza wanafunzi jinsi ya kulima mboga. Mafundisho ya Bwana Shamba yaliwasisimua sana Sima na Shubila. Wakazidi kuvutwa sana na upandaji wa mboga mbalimbali, utiaji wa mbolea na unyunyiziaji wa dawa kwenye miche ili isiharibiwe na wadudu. Wakatambua makosa waliyokuwa wakifanya katika bustani zao. Waliporudi nyumbani walianza kufikiria jinsi ya kupanua kilimo chao cha mboga. Wakaamua kuanza bustani kubwa katika bonde lililokuwa karibu na nyumba yao. Huko wakapanda vitunguu, nyanya na mchicha.
Baada ya haya walichimba mifereji ya kunyweshea bustani zao. Pia walianzisha ufugaji wa samaki. Kilimo kikawapatia fedha nyingi, wakajilipia ada ya shule na kujinunulia nguo na mahitaji mengine. Habari za mafanikio yao ziliwafikia walimu wao. Walimu walifurahi sana. Wakaenda kuangalia kazi walizofanya Sima na Shubila. Siku iliyofuata wakaitisha mkutano wa shule nzima ili kuwaeleza watoto wengine mafanikio ya watoto hao.
Wakawaeleza jinsi watoto hawa walivyoanza kujitegemea. Walimu na wanafunzi walikata shauri kwenda kuona bustani zao pamoja. Walipofika huko walistaajabu sana kuona ustawi wa bustani hizo. Shubila na Sima wakataja kiasi cha fedha walizopata. Wakwaeleza pia kuwa jambo lililoleta mafanikio yao lilikuwa kufanya kazi kwa juhudi na ushirika. Mwisho waliwashauri wanafunzi wenzao wafanye kazi kwa kushirikiana.
Maneno ya watoto hao yalipenya kabisa katika mioyo ya wanafunzi, nao wakawapa pongezi Shubila na Sima kwa juhudi zao. Waliporejea shuleni, wanafunzi wote waliamua kuanzisha bustani za mboga kwa njia ya kushirikiana. Mwalimu Mkuu wa shule ya Iyamba alianzisha Kamati ya Kujitegemea. Ukafanywa mkutano mkubwa wa kuwachagua viongozi. Mkutano huo ulimchagua Shubila kuwa Bwana Shamba. Sima alichaguliwa kuwa Mwandishi, na mwalimu mmoja alichaguliwa kuwa mshauri.
Wanafunzi wengine walichaguliwa pia kuwa waangalizi wa mifugo na bustani. Kisha wanafunzi wote waligawanywa katika makundi manne ya ujamaa. Kila kundi lilikuwa na viongozi wake. Likapewa kuangalia sehemu Fulani ya shamba. Kila kundi likafanya kazi kwa juhudi. Sima na Shubila walisaidia kila kundi. Hawa wawili walikuwa viongozi bora wa shule ya Iyamba katika shughuli za kujitegemea.(P.T)
mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment