
Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya kuwapasha habari wananchi kwa njia ya simu (Breaking News) jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya simu ya Airtel Tanzania, Sunil Colaso. Picha na Cathbert Kajuna.
Dar es Salaam.Kampuni ya Mwananchi Communications Limited,(MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imezindua huduma mpya ya utoaji wa taarifa za papo kwa papo.
Huduma hiyo inayojulikana kama Airtel Mwananchi Breaking News itahusisha utoaji wa habari kupitia wateja wa simu za mkononi wanaotumia mtandao wa Airtel.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Makao Makuu ya MCL, Tabata Relini Dar es Salaam, Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa MCL,Francis Nanai alisema pamoja na mambo mengine, mpango huo unalenga kuwafikishia Watanzania habari sahihi kwa wakati.
Alisema kwa kutambua maendeleo ya teknolojia, matumizi ya simu za mkononi katika kutoa taarifa yanazidi kuongezeka na kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
"Kadri siku zinavyokwenda, teknolojia inaonekana kukua na simu za mkononi kutumika kama njia mojawapo ya kuwasilisha taarifa na kutokana na hilo, MCL kwa kushirikiana na Airtel tumekuja na ushirikiano huu ambao utawawezesha wateja wetu kupata taarifa sahihi na kwa wakati kwa Sh120," alisema Nanai.
Alifafanua kuwa, tangu kampuni hiyo ianzishe utoaji wa taarifa kupitia simu za mkononi, imekwishapata wateja zaidi ya 500,000 ambao wanapata taarifa zinazotokea kila siku papo kwa papo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel, Sunil Colaso alisema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kubuni njia mbalimbali zinazorahisisha utoaji wa huduma za mawasiliano na taarifa kwa wateja wake.
Alisema kupitia huduma hiyo, Watanzania watapata fursa ya kupata habari zinazotokea papo kwa papo kutoka kila kona ya Tanzania, Afrika na Dunia.
"Airtel tuko mstari wa mbele kuanzisha huduma ambazo zinalenga kumrahisishia mawasiliano mteja na kupitia huduma hii ni matumaini yangu Watanzania watapata nafasi ya kupata habari popote walipo," alisema Colaso.
Alisema kwa kuanzia wateja wa Airtel watapata huduma hiyo bure kwa muda wa siku saba na baada ya hapo watatozwa Sh120 kwa siku.
Meneja Masoko wa MCL, Bernad Mukasa alisema taarifa zitakazotolewa kwa wateja wa Airtel zitakuwa katika sehemu tatu; kwamba mteja atakuwa na uamuzi wa kuchagua habari anazozitaka ambazo zitahusisha habari za kawaida, burudani na michezo.
Chanzo, mwananchi
No comments:
Post a Comment