Tuma picha za matukio kwa whatsup +255744268417 Kwa habari tuma kwenye e-mali maishablognews@gmail.com

Tuesday, March 11, 2014

SUMAYE:WATUNZI SAIDIENI KULINDA NDOA


  • Imeandikwa Na   

sumaye19_15410.jpg
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataka Watanzania wenye uwezo wa kuandika vitabu, kujitokeza na kuandika vitabu vitakavyosaidia kuipeleka jamii ya Watanzania mahala stahiki na kulinda maisha ya ndoa.
Alisema hayo mjini hapa jana wakati wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho ‘ Furahia Ndoa’ kilichoandikwa na wachungaji Zakayo na Carol Evelyn Nzogere.
Sumaye alisema kutokana na changamoto za maisha ya Watanzania, vitabu vina umuhimu wa pekee katika kupunguza baadhi ya matatizo katika jamii yakiwemo matatizo ya ndoa.
Alisema maisha ya familia nyingi nchini, yamekuwa yakiharibika kutokana na kutofuatwa kwa misingi bora ya ndoa na hivyo kutia doa mila na desturi za Watanzania.
“Maisha ya familia moja yanapoparaganyika ni doa kubwa katika jamii nzima kwa sababu wale walioharibikiwa watakuwa mzigo kwa jamii nzima na wanaweza kusababisha hata uharibifu kwa familia zilizotulizana. Tukumbuke anayeyakimbia matatizo katika ndoa yake hatujui atakapoangukia. Anaweza kuangukia kwa mtoto wako au hata kwa mwenzi wako.
“Sote tu mashahidi wa ukubwa wa matatizo haya na jinsi yanavyoathiri jamii yetu. Kitabu hiki naamini hata kama hakitayamaliza matatizo haya, kitakuwa cha msaada mkubwa kwa watakaokisoma. Wahenga walisema, “Heri kuzuia kuliko kuponya.”
Mbali na kuwaomba Watanzania kusoma kitabu hicho, aliwaomba watu wenye muda na uwezo kuandika vitabu vinavyoweza kuongoza maisha ya jamii yaende mahala sahihi.
“Aidha niwaombe wale wenye uwezo wa rasilimali lakini hawana uwezo wa kuandika au hawana muda wa kuandika vitabu, basi wawasaidie wale wenye muda na moyo wa kuandika vitabu ili viwasaidie kuwaelimisha Watanzania,” alisema Sumaye.
Sumaye alitaja pia madhara yanayotokana na ndoa kuvurugika kuwa ni pamoja na kuibuka kwa chuki baina ya wanandoa au waliokuwa wanandoa, jambo ambalo wakati mwingine husababisha hata mauaji.
Madhara mengi ni maambukizi ya magonjwa ya zinaa, ikiwa ni pamoja na Ukimwi kwa vile wanandoa hulazimika kutafuta wapenzi nje ya ndoa, ama kwa kutimiza haja ya mwili au kwa kukomoana.
“Lakini pia kuna madhara ya familia kuvurugika na hata watoto kukosa mapenzi ya wazazi na huweza kuhamia mitaani, uchumi wa familia kuvurugika na watoto kukosa mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na elimu.
“Madhara mengine ni kwa watoto kuingia katika uyatima kwa sababu ya urahisi wa moja au wote wa wazazi kufikwa na mauti kwa sababu ya maisha kubadilika,” alisema Sumaye
CHANZO:HABARILEO

No comments:

Post a Comment