
Miaka michache iliyopita wanasoka wengi wenye vipaji vya hali ya juu waliibuka hapa nchini na kuleta tumaini jipya labda watalikomboa taifa lao la Tanzania ambalo kwa miaka mingi limekuwa likihaha kusaka mafanikio katika soka.
Hata hivyo, wakati mashabiki wa soka hapa nchini wakisubiri kuona matunda mema ya wanasoka wao waliojaaliwa vipaji, ghafla mambo yalibadilika kwani wengi wao kutokana na sababu tofauti walishindwa kutimiza matarajio.
Sababu mojawapo iliyoonekana kudhoofisha vipaji vya wachezaji hao ni sifa, yaani wengi wao walionekana kulewa sifa na kusahau kwamba kipaji pekee bila juhudi binafsi hakitoshi kumpa mhusika mafanikio.
Matokeo yake wengi wamepoteza uelekeo na kujikuta wakishindwa kufaidika na vipaji vyao.
Wafuatao ni baadhi ya wachezaji hao ambao pia walibahatika kuichezea Taifa Stars:
Kigi Makasi
Alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' wakati ikifundishwa na kocha raia wa Brazil, Marcio Maximo, pia alikuwa nguzo katika klabu ya Yanga aliyojiunga nayo akitokea kituo cha kuibua na kuendeleza vipaji cha TSA.
Uwezo wake wa kupiga mashuti makali ulimwezesha kuifungia mabao Taifa Stars na hata Yanga.
Hata hivyo, kiwango chake kilianza kushuka siku baada ya siku hadi kufikia hatua ya kutoswa Taifa Stars na baadaye kusugua benchi Yanga. Hata alipohamia Simba alijikuta hapewi umuhimu mkubwa.
Jerryson Tegete
Aliibuliwa na kocha Maximo akiwa kijana mdogo kabisa kutoka Shule ya Sekondari ya Makongo, Dar es Salaam na kuwa mchezaji muhimu wa Taifa Stars.
Kipaji chake cha kufunga mabao kwa umahiri mkubwa kiliivutia Yanga ambayo ilishawishika kumsajili.
Tegete alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga ambao walimsifu kwa umakini wake wa kutumia nafasi chache anazopata kufunga mabao. Bila kutarajiwa, kiwango cha Tegete kilianza kutetereka na kufikia hatua ya kutoitwa katika kikosi cha Taifa Stars, pia amekuwa akisugua benchi katika klabu yake ya Yanga ambayo anaichezea mpaka sasa.
Zahoro Pazi
Akiwa kijana mdogo aliibuka kuwa mpachika mabao mahiri wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kocha Maximo aliyaona makali yake na wakati fulani alimjumuisha katika kikosi chake kilichoshiriki michuano ya Chalenji.
Umahiri wake ulipungua taratibu tangu Maximo alipoachana na Taifa Stars, Pazi hakuwahi kuitwa tena katika kikosi cha timu hiyo.
Baadaye aliihama Mtibwa na kujiunga na Azam FC ambayo nayo aliachana nayo na kuhamia JKT Ruvu aliyoikimbia na kuibukia Simba, lakini kote huko amejikuta akikosa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.
Juma Jabu
Alionekana kama suluhisho la muda mrefu la beki ya kushoto ya Taifa Stars.
Kuitwa kwake Taifa Stars na kocha Maximo kulikuja baada ya kuwika vilivyo na klabu za Ashanti United na Simba.
Kiwango cha Jabu kilianza kuyumba baada ya kuwa anasumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ya bega ambayo yalisababisha anyang'anywe namba na Amir Maftah katika kikosi cha Simba.
Baadaye Simba ilimtoa kwa mkopo katika klabu ya Coastal Union, lakini hakuwika kabla ya msimu huu kujiunga na Ashanti.
chnazo:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment