Tuma picha za matukio kwa whatsup +255744268417 Kwa habari tuma kwenye e-mali maishablognews@gmail.com

Monday, March 3, 2014

WAWAKIRISHI ZANZIBAR WAHOJI BARAZA LEO


salmin-awadh-salmin_41336.jpg
WAKATI Bunge Maalumu la Katiba, likitarajiwa kukutana leo kuamua kura gani itumike katika uamuzi wa mwisho wa kupitisha Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi, wawakilishi wanachama wa CCM, wameibuka na kuhoji maoni ya Baraza la Wawakilishi kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Maoni hayo yalichapishwa jana katika magazeti, yakionesha kuwa Baraza la Wawakilishi limetoa msimamo wa pamoja, kuashiria kutaka muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Mbali na muundo huo, pia inadaiwa maoni ya baraza hilo yalipendekeza Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya nchi na Tanganyika iwe na mamlaka kamili.
Jana Katibu wa Kamati ya Wawakilishi wa CCM, Salmin Awadh Salmin, aliitisha mkutano na waandishi wa habari mkoani hapa na kukanusha kuhusika kwao katika maoni ya Baraza yaliyowasilishwa katika Tume.
Katika mkutano huo wa dharura, Salmin alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliomba taasisi mbalimbali, ikiwemo Baraza la Wawakilishi, kupeleka maoni yake kuhusu Katiba mpya.
Hata hivyo, Salmin alisema walijua kuwepo kwa mwaliko huo, lakini baada ya hapo kilichoendelea kilikuwa siri ambapo baadhi wa wawakilishi wakiwemo viongozi wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi, hawakushirikishwa.
“Ndugu waandishi naomba ieleweke kwamba sisi wawakilishi wa CCM hatukuwa sehemu ya maoni yaliyowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa vile jambo hilo lilifanyika kwa siri bila kutolewa taarifa kwa viongozi wakiwemo viongozi wa Kamati ya uongozi. “Ni jambo la ajabu na kushangaza kuona taasisi yetu kubwa kama hii kuteleza kwa kiasi hicho. Tulitarajia baada ya kuteleza huko, tungepatiwa taarifa ili kutambua kilichotendeka,” alisema.
Alisema walitarajia baada ya kuteleza huko, Baraza lingepatiwa taarifa ili kutambua kilichotendeka, lakini suala hilo halikufanyika.
“Taarifa na maoni hayo yaliyotolewa kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi, hayakuwa na baraka wala hayakuhusisha vikao husika na hivyo kubeba zaidi maoni binafsi ya viongozi waliohusika,” alisema Salmin.
Walioshiriki
Salmin alisema wawakilishi wa CCM wangependa wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine, wachukue nafasi ya kuueleza umma juu ya dhamira na malengo ya kufanya hivyo.
“Natambua pengine mazingira na maono binafsi yalichukua jukumu la kuisemea taasisi na hivyo kutimiza jambo hilo baya na ovu kwa taasisi yetu hiyo bila ya walio wengi kushirikishwa. “Katika uwasilishaji huo, tunasikitika kwa kusema kwamba taasisi yetu hiyo haikutumia fursa ama nafasi hiyo ipasavyo. Ni viongozi wachache tu waliobeba jukumu hili kubwa na zito bila kuwashirikisha wajumbe walio wengi,” alisema Salmin.
Alisema wawakilishi wanashukuru Baraza la Wawakilishi kupatiwa heshima kubwa ya kutoa maoni yao, ingawa utekelezaji wake haukuendana na malengo yaliyokusudiwa.
“Ndugu waandishi tunaendelea kusisitiza kwamba hatukuwahi kukutana wala kuamua kuwasilisha maoni hayo,tunatambua pengine wenzetu hao walikuwa na dhamira njema na pana zaidi hadi kupelekea utaratibu kusahaulika,” alisema.
 CHANZO:HABARILEO

No comments:

Post a Comment